Headlines News :
Home » » KUTOKA MEZA YA TFF

KUTOKA MEZA YA TFF

Written By Bashir Nkoromo on Tuesday, November 20, 2012 | 9:42 AM


*NYAMLANI ATEULIWA KAMATI YA AFCON 2013
*MECHI YA SERENGETI BOYS YAINGIZA MIL 23/-
*UCHAGUZI KAREFA
*MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
DAR ES SALAAM, TANZANIA
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani ameteuliwa kuwemo kwenye ujumbe rasmi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) utakaosimamia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini.

Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou na Kamati yake ya Utendaji. Ujumbe huo wa CAF kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari 10 mwaka huu una jumla ya watu 148.

Nyamlani ni mmoja wa wajumbe watatu watakaoshughulikia masuala ya rufani. Wajumbe wengine ni Prosper Abega kutoka Cameroon na Pierre-Alain Monguengui wa Gabon. Nyamlani ni mjumbe wa Bodi ya Rufani ya CAF yenye watu 12.

MECHI YA SERENGETI BOYS
Mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Congo Brazzaville iliyochezwa juzi (Novemba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 23,021,000.

Mapato hayo yametokana na washabiki 18,022 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 10,000, sh. 5,000, sh. 2,000 na sh. 1,000. Washabiki 15,850 walikata tiketi za sh. 1,000.

Asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 3,511,677.97 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 5,956,635), usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja- pitch preparation (sh. 400,000), Wachina- Beijing Construction (sh. 2,000,000), umeme (sh. 300,000) na ulinzi wa mechi (sh. 3,500,000).

Kwa upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 1,000,537, asilimia 10 ya uwanja sh. 500,269, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 250,134, asilimia 45 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,251,209, asilimia 20 ya TFF (sh. 1,000,537) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 50,027.

UCHAGUZI WA CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU MKOA WA KATAVI (KAREFA)
Mchakato wa uchaguzi wa KAREFA umefutwa kutokana na wagombea watano kati ya nane vyeti vyao vya elimu ya sekondari kuwa na utata. Mchakato wa uchaguzi huo utaanza upya Novemba 21 mwaka huu.

UCHAGUZI WA TASMA
Mchakato wa uchaguzi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) utaanza upya Novemba 26 mwaka huu baada ya mchakto wa sasa kupata wagombea kwenye nafasi mbili tu za Kamati ya Utendaji ya chama hicho.

UCHAGUZI WA CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU MKOA WA RUKWA (RUREFA)
Mchakato wa uchaguzi wa RUREFA utaanza Novemba 26 mwaka huu na Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA itapewa maelekezo ya usimamiaji wa uchaguzi huo baada ya mchakato wa awali kuwa umefutwa kutokana na kufanyika bila kuzingatia kanuni za uchaguzi.

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika keshokutwa (Novemba 22 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 6 kamili mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

Google+ Followers

Total Pageviews

Comments

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. theNkoromo Blog: SPORTS PAGE - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template