Headlines News :
Home » » KUTOKA OFISI ZA TFF DAR ES SALAAM

KUTOKA OFISI ZA TFF DAR ES SALAAM

Written By Bashir Nkoromo on Saturday, November 17, 2012 | 3:03 AM


TAARIFA RASMI:
Katika kikao chake cha tarehe 3 Novemba 2012, Kamati ya Utendaji ya TFF ilipokea taarifa ya mapendekezo ya marekebisho ya Katiba TFF kama ifuatavyo:

Kuingiza kipengele kinachohusu “Club Lincencing” kama ilivyoagizwa na CAF katika waraka wake unaowataka wanachama wote wa CAF, ikiwemo TFF, kuhakikisha kuwa kipengele hicho kinaingizwa katika katiba zao.

Kutokana na ushauri na maagizo ya FIFA, TFF inatakiwa kuunda wa Kamati ya Rufaa ya Uchanguzi (“Elections Appeals Committee”) na kuondokana na utaratibu tulionao hivi sasa ambao Kamati ya Rufaa (“Appeals Committee”) inajigeuza na kuwa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wakati wa mchakato wa uchaguzi wa TFF.

Kuindoa nafasi ya Makamu wa Pili wa TFF pamoja na kutamka kuwa Wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu katika Kamati ya Utendaji watachaguliwa moja kwa moja na klabu zenyewe. Hii inatokana na azimio la Mkutano Mkuu uliopita la kuruhusu uundwaji wa chombo huru cha kusimamia Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza pamoja na kupitishwa kwa Kanuni zinazokiongoza chombo hicho kama zilivyopendekezwa na klabu za Ligi Kuu na kupitishwa na Kamati ya Utendaji.

Baada ya kutafakari mapendekezo hayo, Kamati ya Utendaji ya TFF iliamua kuwa:
Ipo haja ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TFF kama iliyopendekezwa.
Kwa vile mapendekezo mawili kati ya matatu ya ya marekebisho ya Katiba yana uhusiano na Uchaguzi Mkuu wa TFF, ipo haja ya marekebisho hayo kufanyika kabla ya kutangazwa kwa Mkutano Mkuu wa TFF na kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa TFF.
Aidha, kwa vile TFF haina uwezo wa kuitisha mikutano mikuu miwili – Mkutano Mkuu Maalum kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ya TFF; na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi – katika kipindi kifupi kijacho, marekebisho ya Katiba yafanywe kwa njia ya Waraka (“Circular Resolution”). 

Waraka huo (“Circular Resolution”) uwe umeshatayarishwa na Sekretariati ikishirikiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ifikapo tarehe 15 Novemba 2012 na ukabidhiwe kwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaowakilisha Kanda za TFF ambao watahakikisha kuwa  kila Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Kanda husika anapata fursa ya kutoa ridhaa yake.

Zoezi la kupata ridhaa ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu liwe limemalizika katika kipindi cha siku 21. Kikao kinachofuata cha Kamati ya Utendaji kitafanyika Jumamosi tarehe 15 Desemba 2012 kwa madhumuni ya kupokea taarifa ya zoezi hili na kufanya matayarisho ya Mkutano Mkuu. Katiba ya TFF inaelekeza kuwa taarifa ya Mkutano Mkuu itolewe kwa wanachama wake angalau siku 60 (“notice period”) kabla ya Mkutano. Hivyo Kamati ya utendaji inatarajia kuwa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utafanyika Jumamosi na Jumapili ya tarehe 16 na 17 na Februari 2013.

Kamati ya Utendaji ya TFF inasisitiza kuwa utaratibu huu umeamuliwa kutokana na TFF kutokuwa na uwezo wa kifedha wa kutayarisha mikutano mikuu miwili katika kipindi kifupi kijacho. Kinyume chake ni kuchelewa zaidi kufanyika kwa Mkutano Mkuu, jambo ambalo hatuna budi kuliepuka.

Kamati ya Utendaji ya TFF inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wadau wa mpira wa miguu kwa jumla ili kufanikisha zoezi hili na hatimaye kufanikisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TFF.

Wenu Katika michezo, 

Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
KAMATI YA SHERIA, MAADILI NA HADHI ZA WACHEZAJI

Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

Total Pageviews

Comments

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. theNkoromo SPORTS - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template