DK. FENELLA |
NA MWANDISHI WETU
Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara atakuwa mgeni rasmi kwenye mbio za 11 za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika Jumapili tarehe 3 Machi huko Moshi.
Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, waratibu wa mbio hizo alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa Waziri Mukangara ataanzisha mbio hizo zinazotarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka nchi zaidi ya 40 na atakuwa mgeni rasmi katika sherehe ya kutoa zawadi ambapo atatoa zawadi kwa washindi 10 wa mbio za 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon.
“Dk. Mukangara amekubali kuanzisha mbio na kutoa zawadi kwa washindi wa 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa wanaume na wanawake,” alisema Marealle. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Leonidas Gama atakuwa ni kati ya wageni mashuhuri watakaohudhuria tukio hilo.
Marealle aliongeza kuwa Kilimanjaro Marathon ni tukio ambalo limeendelea kuongeza hadhi ya Tanzania kimataifa kila mwaka; na imesaidia kutambua na kutoa fursa kwa wanariadha wa ndani kukua zaidi, kukuza utalii wa Tanzania na watu kupata nafasi ya kufurahi zaidi.
Alisema mbio hizo zitakuwa na viwango vya kimataifa kama ilivyo kawaida na zitasimamiwa na Kilimanjaro Marathon Club, Riadha Tanzania na Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro. Ili kuhakikisha usalama wa wakimbiaji, baadhi ya barabara za ndani na nje ya mji wa Moshi zitafungwa kuanzia saa 12:15 asubuhi hadi 03:30 asubuhi tarehe 3, Machi 2013 ili kuruhusu wakimbiaji kupita salama.
Tanzania Breweries Limited kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro Premium Lager ndio wadhamini wakuu wa Kilimanjaro Marathon na shughuli zingine za burudani baada ya riadha, na wamekuwa wadhamini wa tukio hili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003, juhudi zao katika masoko na matangazo imekuwa mchango mkubwa katika kukuza mbio hizi.
Executive Solutions ni waratibu wa tukio hilo wakati wadhamini wengine ni Vodacom Tanzania (Km 5 Fun Run), GAPCO (Nusu Marathon kwa Walemavu), Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Tanzanite One, New Arusha Hotel, UNFPA, Fastjet na Kilimanjaro Water.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !