Headlines News :
Home » » KUMI WAKATA RUFANI KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF

KUMI WAKATA RUFANI KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF

Written By Bashir Nkoromo on Friday, February 8, 2013 | 9:42 AM


DAR ES SALAAM, Tanzania
RUFANI kumi zimewasilishwa mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika Februari 22 na 24 mwaka huu.

Wakati uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) utafanyika Februari 22 mwaka huu, ule wa TFF wenyewe utafanyika Februari 24 mwaka huu.

Waliowasilisha rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Idd Mtiginjola ni pamoja na waombaji uongozi saba walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho. Warufani hao ni Omari Mussa Nkwarulo na Michael Richard Wambura walioomba kugombea urais na umakamu wa rais.

Wengine ambao waliomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali ni Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Omari Isack Abdulkadir (Dar es Salaam), Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya) na Shaffih Kajuna Dauda (Dar es Salaam).

Warufani wengine ni wadau ambao waliweka pingamizi dhidi ya baadhi ya waombaji uongozi katika TPL Board na TFF, pingamizi ambazo zilitupwa mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa sababu za kiufundi.

Wadau hao waliokata rufani ni Agape Fue dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Jamal Malinzi kugombea urais, Medard Justinian dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Athuman Nyamlani kugombea urais, na Frank Mchaki dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Hamad Yahya kugombea uenyekiti wa TPL Board.

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imetoa siku ya kesho (Februari 9 mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana kwa wote wenye maslahi na rufani hizo (interested parties) kupitia rufani hizo na kuwasilisha hoja zao kwa maandishi.

Kwa watakaoshindwa kufanya hivyo watapata fursa ya kuwasilisha hoja zao kwa mdomo, ambapo wanaweza kuwa wenyewe au wanasheria wao siku ya usikilizwaji wa rufani hizo. Rufani zitasikilizwa Jumapili (Februari 10 mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi.

OLJORO MWENYEJI WA SIMBA VPL 2012/2013
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 inaingia raundi ya 16 kesho (Februari 9 mwaka huu) kwa mechi nne ambapo Oljoro JKT itaikaribisha Simba jijini Arusha.

Mechi hiyo namba 129 itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid huku Simba ikiingia na kumbukumbu ya sare katika mechi yake iliyopita dhidi ya JKT Ruvu wakati wenyeji wao wakiwa wameshinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 3,000 tu utatumika kwa mechi kati ya wenyeji Kagera Sugar na Mgambo Shooting. Mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Amon Paul kutoka Musoma mkoani Mara.

Toto Africans baada ya kufanya vibaya katika mechi tatu zilizopita ugenini imerejea nyumbaji jijini Mwanza itakapoumana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo utaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons na African Lyon ambayo imepata huduma za kocha mpya Salum Bausi kutoka Zanzibar. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa Bausi kuiongoza timu katika VPL.

Maofisa wengine wa mechi hiyo ni mwamuzi msaidizi namba moja Abdallah Rashid, mwamuzi msaidizi namba mbili Abdallah Mkomwa wote kutoka Pwani wakati mwamuzi wa mezani ni John Kanyenye wa Mbeya. Kamishna wa mechi hiyo ni Rashid Rwena kutoka Ruvuma.

Mechi kati ya Mtibwa Sugar na Azam iliyokuwa ichezwe kesho imesogezwa mbele kwa siku moja ambapo sasa itafanyika Jumapili (Februari 10 mwaka huu) katika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.
                     
FDL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao inaendelea kutimua vumbi wikiendi hii kwa mechi kumi na moja zitakazopigwa kwenye viwanja mbalimbali.

Kundi A keshokutwa (Februari 10 mwaka huu) Mbeya City itacheza na Polisi Iringa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Mkamba Rangers itaumana na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Mkamba) wakati JKT Mlale itakuwa mwenyeji wa Kurugenzi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Green Warriors na Ndanda zitacheza kesho (Februari 9 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B. Mechi nyingine kundi hilo kesho ni kati ya Tessema na Villa Squad kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Keshokutwa (Februari 10 mwaka huu) Transit Camp itacheza na Ashanti United kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakati Polisi Dar es Salaam na Moro United zitavaana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Kundi C kesho (Februari 9 mwaka huu) ni Polisi Dodoma vs Polisi Tabora (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Polisi Mara vs Mwadui (Uwanja wa Karume, Musoma), Morani vs Kanembwa JKT (Uwanja wa Kiteto, Manyara) na Rhino Rangers vs Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

Total Pageviews

Comments

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. theNkoromo SPORTS - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template