Meneja wa Idara ya Habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi (katikati) akifuatilia maigizo ya wanafunzi katika hafla hiyo.
Na Thehabari.com
WANAFUNZI mbalimbali kutoka katika baadhi ya shule za Sekondari jijini Dar es Salaam leo wameadhimisha Siku Kuu ya Wapendanao (Valentine Day) kwa mtanzamo wa Kijinsia ikiwa ni
kushinikiza jamii kuadhimisha sherehe hiyo kwa mtazamo tofauti na mazoea kwa siku hiyo.
Wakizungumza katika maadhimisho hayo wengi waliitaka jamii kubadili mtazamo wa maadhimisho ya Valentine na kuijali jamii zaidi isiojiweza kwa kuisaidia kuonesha upendo na kuacha kuegemea katika mapenzi ambayo yamekuwa yakiipotosha jamii.
Mwanafunzi Grace David kutoka Shule ya Sekondari Loyola alisema mapenzi ya kweli hayawezi kuoneshwa kwa mtu kwa siku moja pekee, bali hali hiyo inapaswa kuwepo siku zote tofauti na mtazamo ya vijana wengi wanavyoichukulia 'Valentine Day'.
Naye Meneja wa Idara ya Habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi akizungumza na wanafunzi alisema siku ya Valentine hivi sasa imegeuzwa kibiashara zaidi na jamii kiasi cha kuyaathiri makundi mengine ya jamii kwa namna mbalimbali.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa kadi za ujumbe wa mapenzi zinauzwa kwa kiasi kikubwa siku hiyo ukilinganisha na sikuu kuu zingine, huku biashara nyingine za starehe zikifanywa kiasi kikubwa.
Alisema jamii ina kila sababu ya kuanza kubadilika na kuadhimisha siku hiyo kwa kujitolea kwa makundi yasiojiweza kama watoto yatima, wazee na wajane ambao wanaishi katika mazingira magumu.
Hata hivyo alisema ukatili wa kijinsia na mapenzi umekuwa ukiibuka kwa kasi katika siku kuu hiyo; kama wapenzi (katika ndoa) kuwasaliti wapendwa wao, ukatili wa kimapenzi, vipingo na starehe zisizo na tija jambo ambalo linafanya makundi yasio na uwezo kutengwa.
Aidha aliongeza kuwa wanafunzi nao wamekuwa wakijikuta wakitoka katika maadili yao na kujiingiza katika mapenzi na ngono zembe jambo ambalo limekuwa likiwaathiri kwa kiasi kikubwa.
"Valentine ni maadhimisho ya kumbukumbu ya mwanaharakati aliyekuwa mtetezi wa haki za makundi ya vijana katika jamii ya Ki-nubi ambao walinyimwa haki zao katika masuala ya mahusiano, sasa tunaisherekea kimapenzi zaidi...," alisema Bi. Liundi.
Makundi hayo ya wanafunzi kutoka shule za Sekondari Yusuf Makamba, Loyola (Loyola High School), Mabibo, Perfect Vision na Sinza Tower yamekutanishwa na TGNP kwa kushirikiana na Taasisi ya Soma Book Cafe ya jijini Dar es Salaam.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !