KAMATI ya Utendaji
ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) iliyokutana jijini
Dar es Salaam wiki iliyopita ilikubaliana kufanya mabadiliko makubwa katika Tuzo
za Wanamichezo Bora Tanzania zinazotolewa kila mwaka na TASWA.
Kikao
kilijiridhisha kuwa tuzo za TASWA zina heshima kubwa na wanamichezo hapa nchini
wanazithamini na kuzitegemea kuliko tuzo za aina nyingine zozote.
Lakini kikao
kilikubaliana kuwa pamoja na hayo bado kuna changamoto mbalimbali kuhusiana na
tuzo hizo, hivyo kuna haja ya kuhakikisha zinaboreshwa zaidi ya ilivyo sasa.
Kutokana na hali
hiyo, kikao kiliunda Kamati Maalum ya watu 12 Kusimamia Tuzo hizo, ambayo
itakuwa chini ya uenyekiti wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, Rehure Nyaulawa
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio 100.5 Times FM na ina wajumbe wengine 10
ambao si viongozi wa TASWA, lakini ni waandishi wazoefu wa habari za michezo,
hivyo tunaamini wataleta ufanisi.
Jukumu la kamati
hiyo pamoja na kuandaa mchakato wa upatikanaji wa Wanamichezo Bora wa Tanzania
mwaka 2013 na kupanga tarehe ya kufanyika tuzo hiyo mwaka huu, lakini pia
imepewa mamlaka ya kutazama mfumo wa tuzo ulivyo na ikiwezekana kuubadili kwa
namna itakavyoona inafaa kwa maslahi ya chama na maendeleo ya michezo kwa
ujumla.
Ni nia ya Kamati
ya Utendaji ya TASWA kuona tuzo inakuwa bora na ambayo wadau wa michezo
wataendelea kuiheshimu kwa kila hatua. Hivyo kuamua kuipa kamati hiyo mamlaka
ya kuamua mambo ya msingi katika kuiboresha kwa mipango ya muda mfupi na mrefu.
Licha ya
Mwenyekiti Nyaulawa, wengine walioteuliwa kuunda kamati hiyo na vyombo vyao
katika mabano ni Elizabeth Mayemba (Mwandishi wa Majira), Amour Hassan (Mhariri
wa habari za Michezo-Nipashe), Dominick Isiji (Mhariri wa michezo-The African)
na Rais wa Chama cha Gofu Wanawake Tanzania (TLGU), ambaye pia ni mwandishi wa
habari za michezo wa gazeti la Daily News, Mbonile Burton.
Wengine ni Mahmoud
Zubeiyr (mmiliki bongostazblogspot), Athanas Kazige (Mwandishi Uhuru), Suleiman
Jongo (Mwandishi-Citizens), Angela Msangi (Mwandishi TBC1) na Cosmas Mlekani
(Mwandishi-Spotileo) na Tulo Chambo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Chama cha Riadha Tanzania (RT) na pia Mhariri wa habari za michezo wa gazeti la
Tanzania Daima.
Katibu wa kamati
hiyo atakuwa Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando na kikao cha kwanza cha kamati
kitafanyika jijini Dar es Salaam Jumatatu Machi 24, ambapo kitafunguliwa na
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto, ambaye kwa sasa yupo safarini.
Ahsanteni.
Egbert Mkoko
Kaimu Mwenyekiti
TASWA
19/03/2014
0759-773727
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !