Headlines News :
Home » » BURIANI DEDE, MAZISHI YAKE YAWEKA REKODI

BURIANI DEDE, MAZISHI YAKE YAWEKA REKODI

Written By Bashir Nkoromo on Friday, July 7, 2017 | 5:32 AM

MWANAMUZIKI gwiji wa uimbaji na utunzi wa nyimbo nchini, Shaban Dede (pichani) hatunaye. Amefariki dunia. Ametangulia kwenda kule ambako sote binadamu lazima tufike, isipokuwa kila mmoja kwa siku na wakati wake. Anaandi mwandishi mkongwe wa habari za michezo na Burudani wa Uhuru Publications Ltd, Rashid Zahor

Hatutamwona tena Dede. Hatutaisikia tena sauti yake tamu na murua, ikighani nyimbo mbalimbali za muziki wa dansi, iwe alizozitunga mwenyewe au zile zilizotungwa na wanamuziki wenzake.

Dede alifariki dunia jana, saa mbili asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, ambako alilazwa wiki mbili zilizopita kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Mkongwe huyo amezikwa leo kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam, katika mazishi yaliyoweka rekodi ya kuhudhuriwa na mamia ya watu, wakiwemo wanamuziki wakongwe na wa kizazi cha sasa na wadau wa tasnia ya muziki.

Kabla ya mauti kumkumba, Dede alishazushiwa kifo wiki iliyopita, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, kutokana na tabia mbaya za baadhi ya binadamu kupenda kuzungumzia mambo ambayo hawana uhakika nayo. Ni kama walikuwa wanamchulia.

Kifo cha Dede kimepokelewa kwa mshtuko na majonzi makubwa na mashabiki wa muziki nchini. 

Sio tu kwa sababu wataikosa sauti yake, bali pia watazikosa tungo zake, ambazo zilimpatia umaarufu mkubwa tangu alipokuwa bendi ya Msongo Ngoma, enzi hizo ikiitwa Juwata Jazz, DDC Mlimani Park, Bima Lee na baadaye kurejea Msondo Ngoma miaka minne iliyopita.

Ni kweli kwamba mauti huua mwili wa binadamu ukabaki vumbi tupu kaburini, lakini yale aliyoyafanya hapa duniani, yatabaki kuwa kumbukumbu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kwa miaka mingi.

Ni kwa sababu Dede alikuwa mmoja wa watunzi mahiri wa nyimbo, hasa alipokuwa bendi ya Mlimani Park, ambapo inasemekana alitunga nyimbo zaidi ya 100, akiwa anashika nafasi ya pili nyuma ya Hassan Rehani Bitchuka.

Pia, alikuwa chachu ya ushindani wa kimuziki uliokuwepo kati ya Msondo Ngoma na Mlimani Park, ambapo alikuwa karata muhimu ya ushindi katika kila bendi. Alikuwa anajua nini cha kufanya ili kuwafurahisha mashabiki na kuwapa ile burudani wanayoihitaji.

Kifo cha Dede sio pigo tu kwa familia yake, bali pia wanamuziki wenzake. Wengi wamemuelezea kuwa, bado alikuwa akihitajika kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kutunga na kuimba nyimbo zenye mvuto.

Vilevile ushauri wake uliwasaidia wanamuziki wengi aliowahi kufanya nao kazi katika bendi mbalimbali alizopitia, ikiwa ni pamoja na kuziletea mafanikio makubwa. Ni sawa na kusema mbuyu umeanguka. Hauwezi kuota tena.

“Ninamfahamu Dede kwa kipindi kirefu kwani alikuwa mtunzi mzuri na mtu mwenye mchango mkubwa katika tasnia ya muziki. Nimesikitishwa sana na kifo chake na pengo lake halitazibika kwa urahisi,” alisema Bichuka, alipozungumza na gazeti hili jana, kuhusu kifo cha nguli huyo.

Kiongozi wa sasa wa Mlimani Park, Abdalah Hemba, amekiri kuwa Dede ndiye aliyeibua kipaji chake, ambacho kwa sasa kimemfanya awe mwimbaji mahiri na kiongozi wa bendi hiyo kongwe nchini.

Hemba alisema Dede ndiye aliyemsaidia kuingia katika bendi hiyo na kujulikana kupitia sanaa ya muziki. Kwamba, alikuwa mtambuzi mzuri wa vipaji vya wanamuziki baada ya kuwa nao kwa muda mfupi.

Wanamuziki wengine walioelezea kusikitishwa sana na kifo cha dede ni wakongwe Abdul Salvador, John Kitime na Hussein Jumbe, ambao wameeleza wazi kuwa sio rahisi pengo lake kuzibika..
Dede alijulikana kwa uimbaji wenye kiwango cha juu kutokana na tungo murua, ambazo baadhi zilitokea kuwa gumzo ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa nyimbo za Dede, ambazo zinapendwa na wadau wa muziki wa dansi ni Fumanizi, Kelele za paka hazimzuii mwenye nyumba kulala, Mshenga, Baba mkwe, Amina, Talaka rejea na Kizabinazabina.

Nyimbo hizo na nyinginezo kadhaa, alizitunga wakati akiwa katika bendi ya DDC Mlimani Park kwa muda wa miaka 27, kabla hajarudi katika bendi yake ya zamani ya Msondo Ngoma, mwaka 2014.

Mbali na wimbo wake wa ‘Suluhu’, ambao ulikuwa wa kwanza kuutunga baada ya kurejea Msondo Ngoma, mwanamuziki huyo pia aliitungia bendi hiyo nyimbo kedekede, ikiwemo Fatuma, Umbeya umenichosha, Julekha, Jane, Kuruthumu na Amba, ambazo zilimjengea umaarufu na kujikuta akipachikwa jina la ‘Kamchape’ na ‘Super Motisha’.

Dede alilazimika kurejea Msondo Ngoma kutokana na bendi hiyo kuyumba baada ya kuondokewa na waimbaji wake waliokuwa tegemeo kubwa, tena mfululizo, akianza Suleiman Mbwembwe, Othmani Momba, Ally Muhoja Kishiwa ‘TX Moshi’ na Joseph Maina.

Vifo vya waimbaji hao vilisababisha bendi hiyo kongwe kubakiwa na mwimbaji mmoja pekee nguli, marehemu Maalimu Gurumo, hivyo uongozi uliona kuna kila sababu ya kumrejesha Dede ili kuongeza nguvu. Alikuwa akisaidiana na Eddo Sanga, Juma Katundu na Hassan Moshi.

Bahati kubwa iliyonayo bendi ya Msondo Ngoma ni kwamba, bado inao wapigaji mahiri wa ala mbalimbali za muziki, wakiwemo Saidi Mabera, Abdul Ridhiwan, Zahoro Bangwe, Huruka Uvuruge, Hamisi Mapanga, Ibrahim Kandaya na James Mawila.

Uwezo wake wa kutunga na kuimba haukuishia kwa bendi hizo mahasimu kwani alipotua Bima Lee, mwaka 1983, aliwika kwa nyimbo kama Kipepeo, Bilionea wa mapenzi, Shangwe ya harusi, Zenaba, Kununanuna na Dunia duara.

Dede pia aliwahi kung'ara katika bendi ya Orchestra Safari Sound, ambako alivuma kwa nyimbo kama Nyumba ya mgumba haina matanga, Habari imeota mbawa, Titi na Mariam, kabla ya kurejea DDC Mlimani Park.

Pumzika kwa amani Dede. Mashabiki wa muziki walikupenda, lakini Mungu amekupenda zaidi. Kazi uliyoifanya hapa duniani imetosha na itabaki kuwa kumbukumbu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kwa miaka mingi.

Ni wazi kuwa umeacha mengi ya kujifunza kwa wanamuziki wa sasa. Nayo ni uvumilivu wa kudumu kwenye bendi kwa miaka mingi, kutunga nyimbo zinazogusa hisia na kuimba kwa sauti yenye mvuto
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

Total Pageviews

Comments

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. theNkoromo SPORTS - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template