Headlines News :
Home » » TASWA YAMPONGEZA WAMBURA, MAANDALIZI KUTANO WAKE MKUU WAIVA

TASWA YAMPONGEZA WAMBURA, MAANDALIZI KUTANO WAKE MKUU WAIVA

Written By Bashir Nkoromo on Thursday, October 25, 2012 | 9:02 PM


DAR ES SALAAM, TANZANIA
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinampongeza mwanachama wake Boniface Wambura kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.

TASWA imepokea kwa furaha uteuzi huo wa Wambura ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na inaamini ataendelea kufanya vizuri kama anavyotekeleza majukumu yake ya kazi ndani ya TFF.

Tangu Wambura aanze kazi ya Ofisa Habari wa TFF kumekuwa na mapinduzi makubwa yanayohusiana na mambo ya habari na katika hili waandishi wa habari za michezo nchini ni mashahidi wa hilo kwani amekuwa mtu sahihi kwao na amekuwa na ushirikiano mkubwa usio na kifani kwa wanahabari wenzake.

Kwa vile Wambura ni mwanachama wetu hai wa TASWA, kwa kuteuliwa kwake huko ni faraja kwa chama na tunamtakia kila la heri ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani hiyo ni ishara tosha kwamba kazi yake inaonekana na inathamanika.

Wambura ameteuliwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012, ambapo atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.

Wakati huohuo, Sekretarieti ya TASWA imefikia hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini wa Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao katika tarehe ambayo itatangazwa rasmi.

Kamati ya Utendaji ya TASWA ilikubaliana katika kikao chake mwezi uliopita kuwa Mkutano Mkuu wa TASWA mwaka huu uwe wa aina yake kwa kuwawezesha wanachama kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na ikashauri ikiwezekana ufanyike nje ya Dar es Salaam kama hali itaruhusu.

Kutokana na hali hiyo, kikao kiliiagiza sekretarieti ya TASWA itafute mdhamini wa kufanikisha suala hilo na kwamba kama ikishindikana mkoani ifanyike Dar es Salaam lakini kuwe na mdhamini.

Tayari hilo limefanyika na mdhamini amepatikana, ambapo hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini itakuwa mapema wiki ijayo  na baada ya hapo itatangazwa tarehe rasmi.

Nichukue nafasi hii kuwaomba wanachama ambao hawajalipa ada zao wafanye hivyo kwa kuwasiliana na Mhazini wa chama au Mhazini Msaidizi ili waepuke usumbufu wa kushindwa kuhudhuria mkutano huo.

Nawasilisha
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
25/10/2012.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

Total Pageviews

Comments

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. theNkoromo SPORTS - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template