Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia
kuondoka leo (Mei 26 mwaka huu) usiku kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo
itaweka kambi na kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kwenda Morocco.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
itaondoka saa 5 usiku kwa ndege ya EgyptAir ikiwa na kikosi cha wachezaji 21
chini ya nahodha wake kipa Juma Kaseja.
Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2 mwaka huu itacheza
mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata itaondoka kwenda
Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la
Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini
Marrakech.
Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji wengine wanaoondoka
katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie kambini jijini Dar es
Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni makipa.
Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Aggrey
Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis
Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas,
Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako
na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watajiunga moja kwa
moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu wakitokea Maputo, Msumbiji mara
baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya
huko.
Katika msafara huo
wa Ethiopia benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu),
Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso
(Meneja wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa
tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !