WIKI iliyopita kulifanyika Mkutano Mkuu
wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS) jijini Baku, Azerbaijan.
Mkutano huo ulishirikisha viongozi wa
vyama 116 vya waandishi wa habari za michezo duniani, ambapo Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kiliwakilishwa na Katibu Mkuu,
Amir Mhando.
Katika mkutano huo msisitizo mkubwa
umewekwa kwa nchi wanachama kutilia mkazo program za kuwaendeleza waandishi
chipukizi wa habari za michezo, lakini pia AIPS yenyewe nayo pamoja na Chama
cha Waandishi wa Habari za Michezo Afrika (AIPS-Afrika) vimechukua jukumu la
kusaidia kwa wale watakaokidhi vigezo wanavyohitaji.
Hivyo kila nchi mwanachama itatuma
wasifu wa majina ya wanahabari chipukizi wasiozidi watano, ambao AIPS yenyewe
itaangalia wale watakaofaa na kuwaandalia mafunzo baadaye mwaka huu.
Kwa upande wa AIPS Afrika yenyewe itaendesha
mafunzo kwa wanahabari chipukizi 25, ambayo yatafanyika Morocco, lakini
kipaumbele cha kwanza kitakuwa kwa nchi 16 zitakazocheza fainali za mataifa ya
Afrika mwakani nchini humo na nafasi zingine zitabaki kwa nchi ambazo
hazitaenda Morocco.
Mafunzo ni ya wazi kwa waandishi wowote
chipukizi wasiozidi umri wa miaka 25, hata wale waliopo kwenye vyuo vya
uandishi wa habari wataruhusiwa kuomba. Tanzania imewahi kupata nafasi moja
mwaka 2011, ambapo Mwita Mwaikenda wakati huo akiwa mwanafunzo wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, alishiriki mafunzo hayo yaliyoandaliwa na AIPS akiwa miongoni
mwa Waafrika watatu tu waliopata nafasi hiyo.
Utaratibu kuhusiana na suala hili
utaelezwa vizuri baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA
kitakachofanyika Jumatatu wiki ijayo kujadili masuala mbalimbali.
B: Ziara Uganda
Kulifanyika kikao cha viongozi wa nchi wanachama
wa AIPS ambao wanatoka Afrika Mashariki, ambapo nchi za Burundi, Kenya,
Tanzania na Uganda zilishiriki na kukubaliana kufanyike ziara ya kimafunzo
itakayohusisha waaandishi wa habari za michezo Septemba 25-29 mwaka huu
Kampala, Uganda. Rwanda licha ya kutoshiriki mkutano wa AIPS, lakini
tulikubaliana nayo ialikwe.
Katika makubaliano hayo kila nchi
itakuwa na washiriki wasiopungua 20 na wasiozidi 35, ambapo pia litafanyika
kongamano kuhusiana na masuala mbalimbali ya waandishi wa habari za michezo kwa
ukanda huo na siku ya mwisho litafanyika bonanza la michezo mbalimbali. Taarifa
zaidi za ziara hiyo itatolewa siku za usoni.
C; Ushirikiano wa kimafunzo
Baadhi ya nchi zilizoshiriki mkutano huo wa 77
wa AIPS, zilikubaliana kuanzisha utaratibu wa kubadilishana utaalamu wa
kitaaluma kwa nchi mbalimbali, kwa kuwatoa baadhi ya wanahabari kwenda nchi
zilizo katika makubaliano hayo kujifunza kwa gharama za nchi mwenyeji.
Hata hivyo makubaliano hayo, yataanza
kufanya kazi baada ya kila nchi kupata baraka za Kamati ya Utendaji na kutuma
majibu kwa waratibu kwamba wanaafiki. Kamati ya Utendaji ya TASWA katika kikao
chake kijacho hilo litakuwa moja ya ajenda.
Nawasilisha.
Katibu Mkuu TASWA
07/05/2014
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !