Headlines News :
Home » » MKENYA KUCHEZESHA MECHI YA STARS, ZAMBIA

MKENYA KUCHEZESHA MECHI YA STARS, ZAMBIA

Written By Bashir Nkoromo on Friday, December 14, 2012 | 5:25 AM


*MTIBWA SUGAR YAICHAPA TOTO 3-1 KOMBE LA UHAI
*PONGEZI KWA UONGOZI MPYA DRFA
*CAF: UKAGUZI WA ‘LESENI ZA KLABU’ JANUARI
DAR ES SALAAM, TANZANIA.
Mwamuzi Sylvester Kirwa kutoka Kenya ndiye atakayechezesha mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) itakayofanyika Desemba 22 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kirwa anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) atasaidiwa na Elias Wamalwa na Marwa Range. Waamuzi hao wasaidizi ambao vilevile watatoka Kenya pia wanatambuliwa na FIFA.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari iko kambini hoteli ya Tansoma, na inafanya mazoezi katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na ule wa Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake.

MTIBWA SUGAR YAICHAPA TOTO 3-1
Mtibwa Sugar ya Morogoro leo asubuhi (Desemba 14 mwaka huu) imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Toto Africans ya Mwanza katika mechi ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U20) za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.

Juma Luzio alifunga mabao yote matatu (hat trick) katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam. Alifunga mabao hayo dakika za 44,81 na 88.

Hata hivyo, Toto Africans ndiyo walioanza kufunga katika mechi hiyo ya kundi A. Bao hilo katika michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai lilifungwa dakjika ya 22 na Pastol Makula.

Nayo Simba imenguruma baada ya kuitandika Mgambo Shooting ya Tanga katika mechi nyingine ya michuano hiyo iliyochezwa leo asubuhi kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi. Wafungaji kwa washindi walikuwa Ramadhan Mdoe dakika ya 19, Mohamed Salum dakika ya 77 na Ramadhan Singano dakika ya 89.

Michuano hiyo inaendelea leo mchana na jioni. Mechi ya Ruvu Shooting na Kagera Sugar iliyokuwa ichezwe mchana Uwanja wa Azam, Chamazi sasa itafanyika saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Mechi nyingine za leo ni Coastal Union vs JKT Ruvu (mchana- Karume), African Lyon vs Azam (jioni- Chamazi). Vilevile mechi kati ya JKT Oljoro na Yanga inachezwa leo Uwanja wa Chamazi.

Kesho (Desemba 15 mwaka huu) ni mapumziko, na michuano hiyo itaendelea Jumapili kwenye viwanja vyote viwili- Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na Uwanja wa Azam- Chamazi.

PONGEZI DRFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaupongeza uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Desemba 12 mwaka huu) hoteli ya Mbezi Garden.

Ushindi aliopata Almasi Kasongo aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji unaonesha jinsi ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa DRFA walivyo na imani kwao.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya DRFA ambayo hivi sasa ina kinara mpya, na kwamba ina changamoto kubwa ya kuhakikisha inaendesha shughuli za DRFA kwa kuzingatia katiba na kanuni.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA chini ya Juma Simba na Kamati ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia katiba na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Safu mpya ya uongozi wa DRFA inaundwa na Kasongo (Mwenyekiti), Meba Ramadhan (Makamu Mwenyekiti), Msanifu Kondo (Katibu), Muhsin Said (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF), Benny Kisaka (Mwakilishi wa Klabu), Ally Hobe (Mhazini) na wajumbe Mohamed Shabani, Sunday Mwanahewa na Bakari Mapande.

CAF KUFANYA UKAGUZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litatuma ofisa wake nchini mwezi ujao kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwenye klabu za Ligi Kuu ya Tanzania kabla ya kutoa leseni kwa zile ambazo zitakuwa zimekidhi vigezo vilivyowekwa. Ili klabu ishiriki mashindano ya CAF ni lazima iwe na leseni hiyo.
Kwa mujibu wa CAF, ofisa huyo atakuwa nchini kuanzia Januari 7 mwakani ambapo atafanya ukaguzi huo hadi Januari 14 mwakani. Mbali ya ukaguzi katika klabu, pia ofisa huyo atakagua viwanja vitakavyotumika katika mashindano yake na hoteli ambazo timu kutoka nje zitakuwa zinafikia kabla ya mechi.

Baadhi ya masharti kabla ya klabu kupewa leseni ya CAF ni pamoja na kuwa na ofisi (physical address), uwanja wake wa mazoezi, programu ya maendeleo kwa vijana, sekretarieti ya kuajiriwa, hesabu za fedha zilizokaguliwa (audited accounts) na benchi la ufundi linaloundwa na watu wenye sifa zinazostahili.

Habari zote na Boniface Wambura, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

Total Pageviews

Comments

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. theNkoromo SPORTS - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template