(Picha/Habari na Benedict Liwenga-WHUSM)
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape
Nnauye amewataka Watanzania kujifunza kuwatia moyo Wanamichezo wanaposhiriki
katika michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Wito huo ameutoa jana Jijini Dar es Salaam wakati wa Hafla ya
kuwapongeza na kupokea bendera ya Taifa toka kwa Wanamichezo ambao walishiriki
katika Mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni mjini Rio, nchini
Brazil.
Mhe. Nnauye alisema kwamba, Watanzania ni vizuri wakajifunza
kusema maneno mazuri kwa wanamichezo pindi wanaporejea toka katika Mashindano
mbalimbali ili kuwapa moyo wa kuendelea kufanya vizuri wanamichezo hao huku
akisisitiza kuwa, ni vema ukosoaji ukaendana na ushauri mzuri wenye kujenga
badala ya kulaumu.
Aliongeza kuwa,
Wanahabari nchini wanapaswa kuandika mazuri yanayofanywa na wanamichezo kwani
yana manufaa kwa Taifa badala ya kutafuta maneno yasiyo na tija ya kukosoa mara
kwa mara kwani kuna wavunja moyo wanamichezo.
“Tukijifunza kuandika na kusema mabaya tu ya kuvunja moyo kwa
wanamichezo wetu hii sio sawa sawa, tujifunze kuwatia moyo, na hii ni hatua ya
kwanza na wito wangu kwa Watanzania wote”, alisema Mhe. Nnauye
Alisisitiza kwamba, Watanzania wanapaswa kujifunza kujivunia
vitu vya kwao kwa njia hiyo itakuwa ikiongeza hamasa kwa wanamichezo katika
kujituma kwa manufaa yao na ya Taifa.
Aidha, alisisitiza kuwepo na maandalizi ya mapema kwa
Wanamichezo nchini ili waweze kufanya vizuri zaidi huku akishauri uwekezaji wa
kutosha katika sekta hiyo na kuyataka Makampuni kuwa na tabia ya kuwatumia
Wanamichezo nchini katika kutangaza utalii wa nchi.
Ametoa wito kwa Viongozi wazembe ambao watashindwa kufikia
malengo mazuri katika tasnia hiyo ni bora wakaachia ngazi zao ili kuwapa nafasi
watu wengine wenye uwezo kutekeleza kazi hiyo.
“Nadhani sasa tuanze kukabana kwenye Vyama, ukichaguliwa na
kukawa na mashindano kama haya, ukashindwa kupeleka hata mchezaji mmoja, kazi
yako ya kwanza nadhani ni kijiuzulu”, alisema Mhe. Nnauye.
Awali akitoa taarifa ya Wanamichezo walioshiriki katika
Mashindano hayo, Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Bw. Gulam Rashid
alisema kwamba, Tanzania ilishiriki mashindano hayo ikiwa na Wanamichezo saba,
walimu wa tatu wa michezO ya kuogelea, Judo na riadha ambapo kati yao wachezaji
wa nne walipata nafasi ya upendeleo (Universality).
Alifafanua kuwa, wachezaji wa nne waliofanikiwa kupata nafasi
ya upendeleo ni wale ambao walishiriki katika michezo mbalimbali katika kusaka
viwango, lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kufikia viwango vinavyowaruhusu wao
kushiriki katika mashindano hayo, hivyo kulingana na Sera na itikadi za
Olimpiki zilitaka kila nchi Duniani ambayo ni Mwanachama wa Mashindano hayo
kutoa watu wake, hivyo walitoa nafasi hiyo kwa wale waliokosa kufikia viwango
kuweza kushiriki.
“Nchi ambayo haikuwa na wachezaji waliofikia viwango vya
Olimpiki walipewa nafasi ya upendeleo kwa wanamichezo kuweza kushiriki na kwa
Tanzania tulikuwa na Waogeleaji wa tatu, mchezaji wa Judo na mchezaji wa kike
wa mbio (Marathon) kwa hiyo, huo ndiyo upendeleo ambao wengi hawauelewi ni
upendeleo upi”, alisema Bw. Gulam.
Aidha, katika hafla hiyo, mbali na kukabidhiwa Bendera ya
Taifa toka kwa kikosi hicho cha Wanamichezo walioshiriki katika Olimpiki
2016 mjini Rio-Brazil, Mhe. Nnauye kwa niaba ya Makampuni ya TTCL na DSTV-Multi
Choice aliwapatia zawadi mbalimbali washiriki hao zikiwemo fedha taslimu ambapo
kwa nafasi ya kipekee Mwanariadha Alphonce Simbu ambaye aliibuka katika nafasi
ya tano katika Mashindano hayo amepatiwa Mkataba wa mwaka mmoja wa kuwa Balozi
wa DSTV ambapo kila mwezi atakuwa akilipwa kiasi cha Shilingi milioni moja
pamoja na king’amuzi maalum, huku washiriki wengine wakipewa ving’amuzi na
fedha.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !